ACHANA NA “SIWEZI KUISHI BILA YEYE” KUNAMAISHA BADALA YA YEYE
Hakuna shaka tulio wengi tupo katika uhusiano wa kimapenzi wa mashaka. Hakuna hata mmoja wetu ambaye anaweza kujiaminisha kwa asilimia mia moja kwamba mpenzi wake aliye naye anampenda kwa dhati kabisa au anazuga. Hii inabaki kuwa siri ya anayependa!
Lakini sasa, kuna kitu nilichogundua miongoni mwetu, kitu ambacho tusipokuwa makini nacho tunaweza kujikuta tunajilazimisha kuishi maisha ya huzuni wakati tunayo haki ya kuishi maisha ya yenye furaha. Ukweli ni kwamba, kila mtu anao uhuru wa kupenda kwani maisha bila mapenzi lazima yatakuwa na kasoro.
Lakini sasa, uhuru huo usikufanye ukalazimika kumpenda mtu ambaye anaonesha wazi kutokuwa na mapenzi ya dhati kwako. Waswahili wanasema, mpende akupendaye, asiyekupenda achana naye. Huo ndio ukweli wenyewe hasa linapoingia suala la mapenzi. Hivi utampendaje mtu ambaye hakupendi? Sawa, huwezi kujua kwamba hakupendi kwani huwezi kuufungua moyo wake lakini, kuna dalili za wazi zinazoweza kukudhihirishia kuwa, mtu huyo anakuzingua tu na kutaka kukupotezea muda wako.
Kitu kinachoniuma na ambacho ndicho kimenisukuma kuandika makala haya ni tabia ya baadhi ya watu kung’ang’ania wapenzi ambao wanaonesha kabisa kutowapenda, ukimuuliza kwa nini anamng’ang’ania wakati hapati anachokitaka, anakuambia eti anampenda sana. Jamani ifike wakati tutambue kuwa, kutokea kumpenda mtu na yeye akakupenda kwa dhati ni bahati sana. Wengi wetu tunatokea kuwapenda watu wasiotupenda, matokeo yake ni kuumizwa kila wakati.
Wewe jaribu kuchunguza utabaini walio wengi hawapati mapenzi wanayoyatarajia kutoka kwa wapenzi wao badala yake huishia kilizwa kila mara. Niseme tu kwamba, kanuni ya mapenzi inasema, nipe nikupe, nipende nikupende, niheshimu nikuheshimu. Kama unabaini dalili f’lani f’lani za wazi kwamba mpenzi wako hakupendi usijilazimishe kuendelea kumpenda. Ukifanya hivyo utamfanya aendelee kukunyanyasa.
Share this:
No comments: